Judges 3:12-30

Ehudi

12 aWaisraeli wakafanya maovu mbele za Bwana tena, kwa kuwa walifanya maovu hayo Bwana akamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu dhidi ya Israeli. 13 bEgloni akawataka Waamoni na Waamaleki waungane naye, akaja kuishambulia Israeli, nao wakatwaa Mji wa Mitende
Yaani Yeriko.
14 dWaisraeli wakawa chini ya Egloni mfalme wa Moabu kwa muda wa miaka kumi na minane.

15 eWaisraeli wakamlilia tena Bwana, naye akawapa mwokozi: Ehudi, mtu wa shoto, mwana wa Gera, Mbenyamini. Waisraeli wakatuma kwa Egloni mfalme wa Moabu ushuru kwa mkono wa Ehudi. 16Basi Ehudi alikuwa ametengeneza upanga wenye ukatao kuwili, urefu wake ni kama dhiraa moja,
Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45.
akaufunga upanga huo ndani ya nguo yake kwenye paja lake la mkono wa kuume.
17 gAkamkabidhi ushuru Egloni mfalme wa Moabu, ambaye alikuwa mtu mnene sana. 18Baada ya Ehudi kumkabidhi ule ushuru, wale watu waliokuwa wameubeba huo ushuru aliwaruhusu waende zao. 19Yeye mwenyewe akafuatana nao hadi kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe karibu na Gilgali, ndipo yeye akarudi, akafika kwa Egloni na kusema, “Ee Mfalme, ninao ujumbe wa siri kwa ajili yako.”

Mfalme akasema, “Nyamazeni kimya!” Nao wale waliomhudumia wote wakamwacha, wakatoka nje.

20 hNdipo Ehudi akamsogelea alipokuwa ameketi peke yake kwenye chumba cha juu cha jumba lake la kifalme la majira ya kiangazi, na kusema, “Ninao ujumbe kutoka kwa Mungu kwa ajili yako.” Mfalme alipokuwa anainuka kutoka kwenye kiti chake, 21 iEhudi akaunyoosha mkono wake wa kushoto na kuufuta ule upanga aliokuwa ameufunga kwenye paja lake la kulia, akamdunga Mfalme Egloni tumboni mwake. 22Hata mpini nao ukazama tumboni pamoja na upanga wenyewe, nao upanga ukatokea mgongoni mwake. Ehudi hakuuchomoa huo upanga, nayo mafuta yakashikamana juu ya upanga. 23Ehudi akatoka nje barazani; akamfungia milango ya chumba cha juu na kuifunga kwa funguo.

24 jBaada ya kuondoka, watumishi wakaja na kukuta milango ya chumba cha juu imefungwa kwa funguo. Wakasema, “Bila shaka amejipumzisha kwenye chumba cha ndani cha nyumba yake ya majira ya kiangazi.” 25 kWakangoja hata wakawa na fadhaa, basi wakati hakufungua milango ya chumba, wakachukua funguo na kuifungua. Tazama wakaona bwana wao amelala sakafuni, amekufa.

26Walipokuwa wangali wanangoja, Ehudi akatoroka, akapita hapo kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe na kukimbilia Seira. 27 lAlipofika huko, akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka vilimani, yeye akiwa anawaongoza.

28 mAkawaagiza, “Nifuateni, kwa kuwa Bwana amewatia Moabu, adui zenu, mikononi mwenu.” Kwa hiyo wakateremka wakamfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kuelekea Moabu, wala hawakuacha mtu yeyote kuvuka. 29Wakati huo wakawaua Wamoabu watu waume wapatao 10,000 ambao wote walikuwa wenye nguvu na mashujaa; hakuna mtu yeyote aliyetoroka. 30 nSiku ile Moabu wakashindwa na Israeli, nayo nchi ikawa na amani kwa miaka themanini.

Copyright information for SwhNEN